Send to a friend |
Na Rashid Kejo KWA wakulima wa zao la muhogo wa mikoa ya kusini hususan Mtwara, wanaelewa fika habari ya matumizi mbalimbali ya zao hilo ukiacha kuchemsha, kutafuna au kukaanga kwa ajili ya mlo. Wanaelewa kwamba muhogo si chakula cha kujikimu njaa pekee, bali ni zao linaloweza kutumika kutengeneza bidhaa nyingine za viwandani kama vile biskuti, chips, keki, gundi na mkate. Huko, kuna mradi unaendelea wa kuongeza thamani ya muhogo unaojulikana kama Cava ambao tayari umeshatoa elimu kwa wasindikaji na waokaji juu ya namna ya kutumia unga wa muhogo kutengeneza bidhaa hizo. Unga wake unachanganywa kwa kiwango fulani na ngano katika kutrengenezea bidhaa hizo Taasisi ya Chakula na Lishe, imewahi kukaririwa ikisema kwamba Tanzania inaweza kuokoa kiasi cha dola za Marekani 12 hadi 24 milioni kwa mwaka ikiwa itapunguza uagizaji na matumizi ya ngano kutoka nje kwa asilimia 20 kwa mwaka... “Ikiwa wakulima wa muhogo nchini watafikia kiwango cha kuzalisha tani 300,000 hadi 600,000 za muhogo mbichi, ambao utasagwa na kupata tani 73,000 hadi 146,000 kwa mwaka.” Mmoja wa waokaji mkoani Mtwara, Mussa Hamisi anasema: “Tunachanganya unga wa muhogo na wa ngano kutengeneza mikate… kwa kweli mikate inayotoka ni mizuri sawa na ile ya ngano tupu… kwa kutumia tekenolojia hii muhogo utapata soko kwani tayari matumizi yake yameongezeka tofauti na awali ambako ulikuwa unatumiwa kwa ugali na kutafuna mbichi.” Wakulima wa Mkuranga wamepiga hatua kubwa zaidi. Wameanza kujifunza uokaji wa bidhaa hizo kwa kutumia unga wa muhogo peke yake bila ya kuchanganya na ngano. Mbali ya kutengeneza keki, wakulima hao wanatengeneza mandazi na tambi za muhogo ambazo wanasema zimeanza kupata umaarufu mkubwa kulinganisha na zile za ngano. Asia Omar Nyakilungi na Salma Ali wa Kitongoji cha Mikwasu, Kijiji cha Njopeka Mkuranga wanasema tangu walipopata ujuzi huo wa kupika keki na mandazi kwa kutumia unga wa muhogo wamekuwa wakijipatia kipato kila siku na pia kupunguza matumuzi ya vitafunwa. Nyakilungi anasema amekuwa akipika keki kwa kutumia kilo mbili za unga wa muhogo ambazo zimekuwa zikimhakikishia kipato cha Sh4,000 kila siku... "Nasomesha wanangu kwa kuuza keki hizi pamoja na shughuli nyingine na nina uhakika wa kupata mahitaji madogo madogo ya muhimu." Kwa upande wake, Salma anasema siku hizi halazimiki kununua vitafunwa kila siku asubuhi au kuchemsha muhogo kwa ajili ya chai kwani mandazi na keki anazopita mbali ya kumwingizia kipato, ndizo anazotumia kwa ajili ya kifungua kinywa. Anasema keki hiyo ina virutubisho vyote muhimu kwani huchanganywa na siagi, mayai, maziwa na sugari. Keki hiyo huwa na rangi ya kahawia." Hata hivyo, Nyakilungi anasema soko la bidhaa zao halijawa kubwa vya kutosha kwani tegemeo lao kubwa ni kuuza katika shule ya kijiji chao na zinapokuwa zimefungwa hulazimika kusimamisha biashara hiyo au kuuza kwa kiwango cha chini mno ambacho anasema hakilipi. "Hii ni changamoto kubwa kwani biashara inasimama wakati inapokuwa inahitajika zaidi. Hiki ni kipindi ambacho tunatafuta fedha kwa ajili ya ada na mahitaji mengine ya watoto wetu shuleni na ndicho ambacho hatufanyi biashara." "Naiomba Serikali itusaidie tupate mitaji ili tupanue soko letu na kuwa na uhakika wa kipato kwani tunaamini kwamba keki za muhogo pamoja na mandazi na tambi, vitakuwa na wateja wengi kutokana na ubora wake." Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Veco la Ubelgiji likishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), limeanzisha programu maalumu ya kuwasaidia wakulima wadogo wa kata sita za wilaya hiyo ili waongeze uzalishaji na kujipatia kipato kutokana na zao hilo. Ofisa Biashara na Ujenzi wa shirika hilo, Clarence Chitemi anasema programu hiyo ya miaka sita iliyoanza mwaka 2008 imelenga kutoa elimu ya kilimo bora, usindikaji wa zao hilo na masoko. "Kuna dalili njema za mafanikio. Wakulima hivi sasa wamebadilika, wamejua mbinu mbalimbali za kuandaa shamba mpaka kusindika. Tumekuwa tukiwekeza Sh 500 milioni kila mwaka tangu tulipoanza na matarajio yetu ni kuona wakulima wanakifanya kilimo cha muhogo kuwa cha kibiashara zaidi badala ya kujikimu na njaa." Mbali ya kupika bidhaa hizo, wakulima wanaonufaika na programu hiyo wamekuwa wakinufaika kwa elimu ya kuongeza uzalishaji na usindikaji kwani hivi sasa inachukua muda wa kati ya saa nne hadi sita kuvuna muhogo hadi kupata unga ambao ni mweupe kama ilivyo ule wa ngano ambao huuza kwa wastani wa Sh800 kwa kilo. Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa halmashauri hiyo, Costantine Mboya anasema muhogo ndiyo zao kuu la chakula wilayani humo likilimwa hekta 50,000 na kuzalisha tani 260,000 kwa mwaka, kiwango ambacho anasema ni kidogo kutokana na wakulima wengi kutozingatia kanuni za kilimo bora na matumizi ya zana duni. Anasema elimu wanayotoa chini ya mpango huo, inalenga kuwajengea uwezo wakulima wa kuvuna muhogo shambani na kuusindika hivyo kuuhifadhi kwa muda mrefu bila ya kuharibika. Mtaalamu wa zao la Muhogo katika Wilaya ya Mkurunga, Dereck Samwel anasema katika siku za karibuni, uzalishaji umeongezeka na kufikia tani nane na kwamba lengo ni kufikia 10 hasa ikizingatiwa kwamba kitaalamu, eka moja inapaswa kuzalisha tani 10 mpaka 15. |
No comments:
Post a Comment