Friday, September 10, 2010

Stars yaichanganya Morocco

Stars yaichanganya Morocco  Send to a friend

Mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni Ushindi ya Taifa Stars,Mohamed Dewji
Vicky Kimaro
WAKATI Kamati ya Operesheni Ushindi ya Taifa Stars chini ya mwenyekiti wake Mohamed Dewji inatarajiwa kukutana mara baada ya sikukuu ya Idd, hali ya wasiwasi imeikumba timu ya taifa ya Morocco mwezi moja kabla ya mechi yao ya ugenini dhidi ya Tanzania.

Akizungumza jijini jana, Dewji alisema mikakati iliyopo ni kuhakikisha Stars inashinda mechi zake zote za nyumbani ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu mashindano hayo."Tutafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha Stars inapata pointi zote tisa za nyumbani na haipotezi mechi yoyote ya ugenini, kwa sasa kamati yangu itakaa kupanga mikakati mbali mbali ya kuhakikisha inaiua Morocco,"alisema Dewji.

Alisema mikakati watakayopanga ni kuhakikisha timu inakuwa kwenye mazingira mazuri na kupata huduma zote zinazostahili, kuwaandaa wachezaji kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha.

"Kuandaa timu ni gharama kubwa, tutakutana baada ya sikukuu hii ya Idd kuangalia jinsi ya kubeba gharama za kuhudumia timu, kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kufanikisha Stars inashinda mechi zake zote na kufuzu,"alisema Dewji.

"Mechi ya Algeria tulionewa sana, hakuna mtu ambaye alitazama mechi ile atapingana na mimi, tutapanga pia mikakati ya kuhakikisha timu yetu haionewi, na tutaipigania hadi tone la mwisho..., Licha ya kuonewa, lakini matokeo tuliyopata yamedhihirisha ukomavu wa timu yetu katika soka, ni wazi wachezaji wetu walienda wakiwa wameandaliwa kiakili ili kukabiliana vilivyo na hali ya uonevu."

Stars ilipata sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Algeria kitendo ambacho kiliwaduwaza mashabiki na benchi zima la ufundi la Algeria na kupelekea kocha wao Rabah Saadane kujiuzulu.

Kutokana na hali hiyo ya kocha wa Algeria kujiuzulu na Morocco kuanza mechi yake kwa suluhu walipocheza na Jamhuri ya Afrika ya Kati , mashabiki wa soka wa Morocco wameingiwa wasiwasi na kusababisha kocha wa muda wa Morocco, Dominique Cuperly kuwataka mashabiki wake kuondoa hofu na kwamba Simba wa Atlas watasonga mbele.

Mfaransa huyo alilimbia gazeti la Le Matin kuwa japokuwa anachukua mzigo wote wa matokeo ya suluhu ya Simba hao dhidi ya Afrika ya Kati, wananchi wa Morocco ni lazima wawe watulivu na waiunge mkono nchi yao katika kipindi chote cha michezo hiyo ya kufuzu kwa fainali za 2012.

“Tunatakiwa kuangalia mbele kwa ushirikiano wa pamoja kwa sababu tutakuwa ugenini kucheza na Tanzania, nimechukua jukumu lote la matokeo dhidi ya Jamhuri y a Afrika ya Kati.

"Nimesoma mengi kutoka kwenye vyombo vya habari wakitulaumu, lakini wanatakiwa kuangalia kwa makini hali yetu ya sasa,” alifafanua.

“Tunahitaji muda wa kujenga upya timu ya ushindani huku tukitilia mkazo kwamba tayari tumeshaanza kampeni ya kufuzu kwa AFCON 2012, Timu haiwezi kujengwa kwa siku moja, hususani ukizingatia kwamba wachezaji hawa hawajacheza pamoja kwa miezi mingi.”

Cuperly aliongeza kuwa Morocco ina wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kutengeneza timu bora, lakini wanahitaji benchi la ufundi bora na kuwachanganya wachezaji wengine kama Mehdi Carcela, ambao wameonyesha moyo wa kutaka kuitumikia nchi yao.

“Tumeongea naye na wachezaji wengine waliosema wanataka kuichezea Morocco, kwa sasa tunaimarisha benchi la ufundi zaidi na kuhakikisha tunapata mtu bora,” alisema mtu pekee anayesubiliwa kuwasili ni Eric Gerets.


No comments:

Post a Comment