Saturday, September 4, 2010

K-LYINN: UREMBO SIO SURA NA MAUMBILE TU

Jina lake halisi ni Jacqueline Ntuyabaliwe, nyota yake ni Sagittarius (Mshale). Wengi bado tunamkumbuka kama mrembo aliyetwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2000 na kisha kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya mrembo wa dunia (Miss World) yaliyofanyikia nchini Uingereza na Visiwa vya Maldives.

Tofauti na mawazo ya wengi, kama anavyobainisha katika mahojiano tuliyofanya naye hivi karibuni, alianzia kwenye muziki kisha akaja kwenye urembo na baadaye akaamua kurejea katika muziki mahali ambapo ndipo alipo hivi sasa. Mwezi ujao anatarajia kufyatua albamu yake ya pili itakayokwenda kwa jina la K-Lyinn- Crazy Over You.
Ametoka wapi, nini mtazamo wake kuhusu muziki na urembo, wapenzi wa muziki na mashabiki wake watarajie nini katika albamu yake mpya, nini siri ya urembo wake na anatoa ushauri gani kwa wasichana? Hayo yote na mengineyo ameyaweka bayana katika mahojiano yafuatayo;
BC: Unaweza kuwaambia mashabiki wako kuhusu maisha yako ya utotoni? Unakumbuka nini kuhusu utoto wako?
K-LYINN: Utotoni nakumbuka jinsi nilivyokuwa nacheza na baba akirudi kutoka kazini na mara nyingi alikuwa akinipeleka kutembea jioni.Pia nakumbuka nilivyokuwa nikienda kanisani na mama.Nilikuwa napenda sana kusomewa hadithi za vitabu.
BC: Historia ya maisha yako, kama ilivyoandikwa kwenye tovuti yako, inaonyesha kwamba baada ya shule ulianza shughuli za muziki kwa kuwa mwimbaji wa Tanzanite Band. Baada ya hapo ukaingia kwenye masuala ya ulimbwende ambapo ulifanikiwa kushinda taji la Miss Tanzania mwaka 2000 na kisha baadaye ukarejea kwenye muziki tena. Nini kilivutia kwanza kuingia kwenye muziki na kisha masuala ya ulimbwende?

K-LYINN:
Tokea nilipokuwa na miaka sita au saba nakumbuka nilikuwa napenda sana kuiga na kuimba nyimbo za wanamuziki wa ulaya kama Madonna na Mariah Carey,kwahiyo nilipopata nafasi ya kujiunga na bendi ya Tanzanites kwangu ilikuwa kama njia ya kutimiza ndoto yangu.Kuhusu urembo nakumbuka kuna wakati nilikuwa natamani nipate nafasi ya kuvikwa taji na kuwakilisha nchi yangu lakini sana sana niliamua kushiriki baada ya kukutana na watu mbalimbali ambao walinishawishi nishiriki na kunipa moyo kuwa nina nafasi ya kushinda.
BC: Nini siri ya urembo wako?
K-LYINN: Kwanza kabisa mimi binafsi napenda sana kujipatia muda mrefu wa kupumzisha akili na viungo kila siku na kupata usingizi wa kutosha na ninaamini hiyo ni siri mojawapo ya urembo.Pia huwa nakunywa maji mengi na kula matunda na mboga katika mlo wa kila siku.Nikipata muda huwa nafanya mazoezi.
BC: Miaka zaidi ya sita sasa imepita tangu ulipovishwa taji la Miss Tanzania. Unaweza kutukumbusha kidogo ulijisikiaje siku hiyo?
K-LYINN: Kwanza nilitangazwa kuwa mshindi nakumbuka kuwa nilishikwa na butwaa na ilichukuwa muda kuamini ni mimi niliyeshinda na baada ya kuamini nilijisikia furaha isiyo na kifani.
BC: Mafanikio uliyoyafikia kwenye masuala ya urembo ni ndoto ya wasichana wengi sana.Je pamoja na muziki bado unajishughulisha na masuala ya urembo? Kama ndio kwa jinsi gani na kama hapana, kwanini umeacha?
K-LYINN: Kwa sasa huwa sijishirikishi sana na masuala ya urembo kwanza kwasababu kazi ya muziki inachukua muda wangu mwingi,lakini pia ni kwasababu bado hatuna kazi nyingi sana hapa kwetu zinazohusu urembo.
BC: Unaye mtu yeyote ambaye unamuona kama role model wako? Kwanini?
K-LYINN: Baba yangu ni role model wangu,ni mtu mkarimu na yeye ni daktari na amejitolea maisha yake kusaidia watu.Pia naamini ni baba mzuri sana kwasababu bahati mbaya mama yangu alifariki miaka kumi na mbili iliyopita na baba alinilea vizuri mpaka nimefikia hapa nilipo.Yeye huwa tayari kunisikiliza muda ninapohitaji kuongea nae na huniunga mkono na kunipa ushauri katika maisha yangu.

BC: Sasa naomba tuongelee albamu yako mpya unayotarajia kuitoa hivi karibuni.
Kwanini umeamua kuiita albamu hii K-LYNN?
K-LYINN: Album yangu inaitwa K-LYINN CRAZY OVER YOU,Nimeamua kuuita hivyo kwasababu napenda watu walifahamu na kulizoea jina langu na Crazy Over You ni jina la single itakayokuwepo katika album yangu.
You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video
BC: Je unatunga mashairi ya nyimbo zako zote wewe mwenyewe?
K-LYINN: Ndio,mashairi yote utakayosikia katika album yangu nimetunga mwenyewe.
BC: Watu wengi wangependa kufahamu, inakuchukua muda gani kutengeneza albamu nzima kama hii yako?
K-LYINN: Muda wa kutengeneza album huwa unatofautiana,lakini album hii imenichukuwa mwaka mmoja kuikamilisha.
BC: Itakuwa na nyimbo ngapi kwa ujumla na imerekodiwa katika studio gani?
K-LYINN: Album itakuwa na nyimbo kumi,nimefanya kazi na producers tofauti kama Said Comorian,Mwaks,Dunga na Roy.
BC: Katika albamu hii mpya utakayoitoa hivi karibuni umewashirikisha wasanii gani?
K-LYINN: Album hii nimemshirikisha Mr.Blu,Sweeza,na Noora.
BC: Wapenzi wa muziki wategemee nini kipya katika albamu hii?
K-LYINN: Wapenzi wategemee ujumbe utakaowagusa na mziki utakaowafanya waamke na kucheza.Album hii niliitengeneza kwa ajili ya mashabiki wangu.
BC: Nyimbo zako nyingi katika albamu iliyopita zilikuwa zinahusu masuala ya mapenzi. Wengi tungependa kujua, kwanini unapenda zaidi kuimba nyimbo za mapenzi? Hadithi zilizoko kwenye mashairi yako zinatokana na uzoefu wako binafsi?

K-LYINN:
Napenda kuimba nyimbo tofauti tofauti na lakini kwa sasa naamini nyimbo za mapenzi zinagusa rika tofauti na kuna mambo mengi ya kuimba katika masuala ya mapenzi na zina wapenzi wengi sana,pia katika album hii mpya kuna nyimbo isiyo ya mapenzi.Hadithi zilizoko katika nyimbo zangu zinatokana na hadithi zinazotokea katika maisha ya watu tofauti sio hadithi zangu binafsi.

BC: Mara nyingi wasanii wa muziki huwa wanakuwa na malengo maalumu katika miziki wanayotunga, kuiimba na hata kucheza. Kwa miaka mingi makundi mawili makubwa yamekuwa ni wale wanaofanya muziki kwa ajili ya kuelimisha na wanaofanya kwa ajili ya kuburudisha. Muziki wako upo zaidi katika kundi gani kati ya haya?
K-LYINN: Nafanya muziki kwa ajili ya kuburudisha na kuelimisha kwa ujumla.
BC: Nini maoni yako kuhusu muziki wa kizazi kipya ambapo katika siku za hivi karibuni umekuwa ukizungumziwa kama muziki utakaopita haraka kutokana na kukosa ujumbe wa maana?
K-LYINN: Mimi naamini mziki wa bongo flavour unaweza kufananishwa na mziki wa R&B na mziki usioweza kupita kwani aina ya mziki huu hubadilika kutokana na wakati,si kweli kwamba mziki huu hauna ujumbe kwasababu ziko nyimbo nyingi sana ambazo zina mashairi yenye ujumbe wa maana ila labda mwelekeo wa sasa asilimia kubwa ni nyimbo za mapenzi kwasababu inaonekana kuwa zina wapenzi wengi lakini msanii mwenye kipaji anaweza kubadilika na kutunga mashairi yenye maudhui tofauti inapohitajika.
BC: Ukiacha wewe mwenyewe, ni msanii au wasanii gani duniani wanaokuvutia sana na ambao ungependa kufanya nao kazi siku za mbeleni?

K-LYINN:
Namzimia sana Beyonce na Mary J Blige,kwa wasanii wa kiume ningependa
kufanya kazi na Usher Raymond,Neyo,Basta Rymes na Jay Z.
BC: Mbali ya Tanzania umewahi kufanya perfomances katika nchi gani zingine? Huwa unajisikiaje kuperfom nje ya Tanzania?
K-LYINN: Nimeshawahi kufanya performances nje na bendi,na kwa ajili ya kuitangaza album yangu ninapanga kufanya tour katika baadhi ya nchi za Africa na UK na US pamoja na baadhi ya nchi za Europe.Ratiba za shows zitapatikana katika website yangu www.klyinn.com
BC: Unatoa ushauri gani kwa wasichana wadogo wanaotaka aidha kuingia kwenye mambo ya urembo au muziki? Nini tofauti kati ya fani ya muziki na urembo?
K-LYINN: Wasichana wanaopenda kuingia katika masuala ya urembo nawaambia kuwa kwanza wasome na wasubiri kufikia umri unaotakiwa,urembo sio sura na maumbile tu bali pia ni ufahamu na mambo mengi mengine huwa yanayotakiwa.Na ili kufanya muziki ni muhimu kuwa na kipaji asilia na kama wanaweza kusomea fani hiyo wataweza kufanikiwa zaidi kwani muziki ni kama biashara ambayo kama unaifanya vizuri unaweza kuitumia kuendesha maisha.
BC: Kwa wapenzi wa muziki ambao wangependa kununua albamu yako unawaambia nini? Nani msambazaji wako na itapatikana katika maduka gani?
K-LYINN: Wapenzi wa muziki wangu watakaopenda kununua album yangu napanda kuwaambia kuwa album yangu ikishatoka watapata taarifa za mahali au maduka zitakapokuwa zikiuzwa katika matangazo na vile vile katika website yangu WWW.KLYINN.COM.
BC: Asante K-Lyinn kwa mahojiano haya na kila la kheri.
K-LYINN: Asanteni pia.

No comments:

Post a Comment