Saturday, September 4, 2010

Ujumbe wa simu wazua hofu


 Send to a friend



Richard Kihiyo
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watumiaji wa simu za mikononi kupuuza ujumbe wa tahadhari ulioanza kusambazwa jana na watu wasiojulikana, ikisema kuwa ni uzushi.
Jana kulikuwa na aina mbili za taarifa za tahadhari zilizokuwa zikitumwa kwa wateja wa simu za mikononi. Ujumbe wa kwanza unasema: “Ukipigiwa simu kwa private no (namba binafsi). au ikiandika call kwa red colour (rangi nyekundu) usipokee, ni mionzi, utapalarize (utapooza) na kufa.
Imetokea Kenya watu wamekufa. Julisha ndugu na jamaa wote.” Ujumbe mwingine unawataka watumiaji wa huduma hiyo wasipokee simu yoyote watakayopigiwa kupitia namba 7888308001, 9316048121, 9876266211, 9888854137 na 9876715587.
Ujumbe huo unasema: "Namba hii inapigwa na rangi nyekundu, unaweza kupata brain damage (tatizo la ubongo) kwa kupokea simu.
Watu 27 walifariki mara tuu baada ya kupokea simu iliyopigwa kutoka katika namba hizo." Ujumbe huo ulisababisha watumiaji wa simu kuingiwa na wasiwasi na baadhi waliwasiliana na chumba cha habari cha Mwananchi Communications kutaka ufafanuzi wa suala hilo na wengine wakieleza hofu ya kupooza.
Hata hivyo, taarifa iliyotumwa na msemaji wa TCRA, Innocent Mungy ambayo imesainiwa na kurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, Profesa John Nkhoma, inasema: “Ujumbe huo unatakiwa kupuuzwa kwa kuwa ni uzushi usuokuwa na ukweli wowote.” Kutokana na ujumbe huo kusambazwa kwa watu wengi, TCRA imesema hakuna ukweli na hivyo kuwataka wananchi kuupuuzia. "Mamlaka ya Mawasiliano inapenda kuwahakikishia wananchi kwa ujumla kwamba taarifa zinazoenezwa ni za uzushi na sio za kweli.
Wananchi wanaombwa kupuuza uzushi huo kwa kua hauna ukweli wowote," inasema taarifa hiyo ya TCRA.
Ilifafanua kuwa kutokanha na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna tafiti nyingi zimefanyika sehemu mbalimbali duniani ambazo zimeonyesha kwamba kiwango cha mawimbi ya mawasiliano hakina madhara kwa afya ya binadamu. 
TCRA iliwataka wote kuendelea kuwa na imani na teknolojia mpya zikiwemo za mawasiliano ya simu, utangazaji na utumiaji wa kompyuta ambazo zinatumiwa ulimwenguni kote bila madhara yoyote. "Madhumuni ya Mamlaka ya Mawasiliano na watoa huduma za mawasiliano kwa ujumla ni kuwaletea wananchi wa Tanzania mawasiliano bora kwa kujenga miundombinu, kutoa huduma bora na matumizi mema," inasema sheemu ya taarifa hiyo.
Mmoja wa watumiaji wa simu za mkononi, Frank Kimboyi ambaye naye alitumiwa ujumbe huo, alisema mwanzoni alipata wasiwasi mkubwa. "Baada ya kuupokea kidogo nilishituka, lakini baada ya kukaa na kutafakari uwezekano wa kitu kama hicho kutokea niliona ni mdogo na nikaamua kuupuuzia," alisema Kimboyi.

No comments:

Post a Comment